Njaa na Kilio cha Neymar, Shibe ya Kulevya ya Messi na Iniesta
Wakati mchezo kati ya Barcelona dhidi ya Juventus ukiendelea wengi walikuwa wanatizama na kusikiliza filimbi ya mwamuzi Bjorn Kuipers itaaamua nini. Wengi walikuwa wanasubiri baraka za waamuzi na namna zinavyofanya kazi na vilabu vya Hispania na wengi walikuwa wanasubiri maajabu mapya wa Barcelona baada ya yale yaliyofanyika kwa PSG.
Kwenye kichwa chake Neymar aliamini inawezekana, kwenye moyo wake Messi aliamini ni bora zaidi na angeweza, kwenye imani yake Suarez aliamini ni mhuni sana na angeweza kusababisha yote yawezekane. Unazungumzia klabu iliyofunga amabao 3 ndani ya dakika 7 dhidi ya PSG iliyokuwa imejihakikishia kufuzu mpaka dakika ya 85 ya mchezo wa pili.
Imani kwenye mioyo ya mashabiki ilikuwa kubwa na ndio maana haikuwa ajabu kuona mmoja wao akiwa na abango lililoandikwa Safari Kuelekea Cardiff ilikuwa bado inawezekana. Hizi ni fikra ambazo zilimfanya Simao Sarbrosa kuamini Anfield ulikuwa uwanja wa kipekee kwa mashabiki kutokukata tamaa.
Benfica walikuwa wameiondoa Liverpool na washabiki wake wa wakati huo walikuwa wakiimba muda wote achana na hawa wa sasa wanaomkimbia Klopp uwanjani mechi inapokuwa imekwenda kombo. Hiki ni kitu kinachotengenezwa na kocha na wachezaji kisha washabiki wanaamini ndani yake, akiibuki ghafla. Barcelona waliandika tayari.
Aliyeongoza hili bahati nzuri alikuwa ni kijana bishoo tu, kijana ambaye ugumu haukuwahi kuwa jadi yake na kijana ambaye muda wote angependa kucheza ili akukere, anaitwa Neymar. Sio Messi kama ambavyo wengi wangeweza kutegemea, huyu amekuwa silaha yao msimu huu hata asipofunga, anarahisisha kazi ya Barcelona kwa kiasi kikubwa sana.
Inawezekana usiweze kumlaumu Messi kwa sababu ametumika kwa nguvu kubwa tangu akiwa na umri mdogo, hana tena muda wa kuibuka na mbinu mpya mambo yanapokuwa kombo kwa sababu nyingi alizitumia akiwa kijana. Kwa sasa Messi ni kama Askofu tu, hafanyi misa nyingi lakini akifanya inakuwa kubwa zaidi na wala hajisumbui sana. Neymar ndiye paroko ama mchungaji wao na anatoa mahubiri yote kwa sasa.
Huu ni wakati wake na Barcelona wanatizama anachokifanya timu ya Taifa na wanaridhika. Lakini kuna tofauti moja kati ya Barcelona na timu yake ya taifa. Pamoja na kuwa ni mchezaji wao muhimu kwa sasa, bado Barcelona hawajaamua kukubali kuondoa makali ya upanga wa Messi kwa kiasi kikubwa, naam Messi huyu ambaye hana kasi yake tena na hawezi kuuamua mchezo kutokea katikati.
Inakuwa rahisi zaidi timu kumuwinda Neymar kwa sababu wachezaji wengine wanasubiri atende, ili wanufaike. Kipindi cha Nyuma, dawa ya MSN ilikuwa haikupatikana na eneo la kiungo lilikuwa bora hivyo hawakuzuilika. Msimu huu eneo lao la kiungo limekumbwa na ukame na mwenye rutuba amebaki kuwa Sergio Busquets peke yake. Huyu ambaye alienda kumpokea Neymar aliyekuwa analia na kumpeleka kwenye vyumba vya kubadili nguo.
Ndani ya Barcelona kuna Messi atakayefikisha miaka 30 mwezi Juni akiwa ameshachukua kila alichotaka ndani ya Barcelona zaidi ya mara tatu, Kuna Iniesta ambaye hana haja ya kujifunza mbinu mpya, Suarez ambaye haufahamu utamaduni wa hapo na ambaye unaweza kukubali hawakilishi nembo yao kwa kiasi kikubwa na Sergio Busquets aliyeshinda kila kitu akiwa bado kijana.
Hivyo uti wa mgongo wa Barcelona wote una ugonjwa mmoja isipokuwa kwa Neymar. Wote wameogelea dimbwi la mafanikio na wote wamejikuta wanazeeka kabla ya umri wao na wala hawajisumbui kuhangaika sana. Katika hili Neymar atakuwa yatima, atalia peke yake na Messi hatojali sana. Kilio cha Messi kwenye Copa America baada ya kukosa Penalty hawezi kukitoa tena Barcelona, kule timu ya Taifa bado ana deni.
Neymar anaamini baada ya Messi na Ronaldo anafuata yeye. Anaamini kuwa hakuna kijana wa umri wake kushuka chini anayeweza kufanya anayoyafanya, ambaye anaweza kuamua maisha ya timu ya Taifa na klabu kwa ujumla kama yeye. Hii ni akili aliyojengewa tangu akiwa Santos mpaka timu ya taifa na kisha Barcelona na ndio iliyomkomaza kuliko wachezaji wengine wa umri wake kama Hazard, Dybala, Griezmann na hata Bale.
Kilio chake dhidi ya Juventus kilikuwa na ujumbe. Alikuwa ndiye mchezaji anayeuhitaji ushindi kuliko wengine kwenye kikosi cha Barcelona. Unaweza usimlaumu Suarez, lakini Messi na wengine wameshiba ndani ya klabu, matumbo yamejaa na la Neymar peke yake bado lina nafasi kubwa. Bado anautamani mpira na bado hajaweza kutwaa uchezaji bora wa dunia.
Barcelona hawajawa tayari kumbebesha timu, sio kwa sababu hastahili lakini kwa sababu wataanzaje kuitoa kwa Lionel Messi ambaye bado ana uwezo wa kufunga mabao mengi zaidi ya Neymar na Suarez kwa sababu bado timu imemzunguka yeye? Neymar ana njaa, Messi ana shibe, Iniesta na Busquests wamevimbiwa kabisa.
Bahati mbaya hata Usajili wao umekuwa mbaya msimu uliopita, hawakuleta mtu ambaye anaweza kuamua matokeo nje ya waliokuwepo. Sio Paco Alcacer wala Gomez au Dennis Suarez wanaoweza kuamua timu ishinde inapohitajika. Msimu ndio umekwisha kwa Neymar kwa sababu hata El Clasico hatokuwepo, hatopata sehemu ya kuonyesha Ulimwengu maajabu ya PSG.
Kilio chake dhidi ya Juventus kilikuwa chake peke yake, na ndio maana aliyemsaidia kulia alikuwa Mbrazil mwenzie na mpinzani wake kwa usiku huo Dani Alves. Huyu alimpa kumbatio la kiundugu tu. Najua msimu ujao atakuja tofauti, atakuwa mchoyo ikibidi, atakuwa hatari kivyake huku pia akikumbatia uwepo wa MSN. Hivyo ndivyo Messi alivyofanikiwa, pamoja na uhatari wa Barcelona alijijenga kuwa hatari zaidi ndani ya mchanganyiko huo.
Pole Neymar kilio kilikuwa chako peke yako, njaa ilikuwa yako peke yako, Suarez hawezi kupewa hii timu, yeye ataendelea kuwa kiungo muhimu kwenye pishi hili. Bahati mbaya kwako Messi kashashiba, msimu ujao njaa yako ikuongoze, kilio chako kikuongoze huku ukinufaika na Messi kujazilizia sehemu ya wazi ya tumbo iliyobaki. Kwa kiasi kikubwa mwezio keshashiba, akina Iniesta ndio kabisa kwa sababu wana mpaka Kombe la dunia, shibe imewalevya.
Post a Comment