TAARIFA KWA UMMA KUHUSU VIFUNGASHIO VYA POMBE KALI – VOROBA
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January
Mamkamba. (MB) akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya uzalishaji,
uingizaji , usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya plastiki maarufu
kama viroba vinavyotumika kufungashia pombe kali, alipozungumza na
waandishi wa habari Ofisini kwake Mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam
Leo.
Katikati
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.
January Makamba. (MB) akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya
uzalishaji, uingizaji , usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya
plastiki maarufu kama viroba vinavyotumika kufungashia pombe kali, kulia
ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Profesa Faustin Kamuzora na Kulia ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira, Waziri Makamba alizungumza na
waandishi wa habari Ofisini kwake mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam
Leo.
Mtakumbuka
tarehe 20 Februari 2017 Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa tamko la
Serikali la utaratibu utakaotumika kutekeleza agizo la kusitisha
utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zinazofungashwa kwenye
vifungashio vya plastiki (viroba)kuanzia tarehe 1 Machi 2017.
Utekelezaji wa katazo hili utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria
ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu
230 (2) (f) cha sheria hiyo, na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya
mwaka 1968 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2012.
Napenda
kusisitiza na kuujulisha umma wa Tanzania kuwa utekelezaji wa maamuzi
haya ya Serikali kuhusu usitishaji uingizaji, uzalishaji, uuzaji na
matumizi ya vifungashio vya plastiki vya kufungia pombe kali utaanza
rasmi tarehe 01 Machi, 2017, katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Operesheni
ya kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la usitishaji utengenezaji,
uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya
plastiki itaendeshwa nchini kote kuanzia tarehe 2 Machi 2017 kwa kupitia
Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira katika ngazi ya
Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na Mtaa. Kamati hizi zitawajibika
kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na nakala Ofisi ya
Makamu wa Rais.
Mnamo
terehe 24 Februari 2017, kiliitishwa kikao cha Mawaziri na viongozi wa
taasisi za Serikali kujadili mpango wa utekelezaji wa zuio hili. Katika
kikao hicho, Wizara na taasisi za Serikali zilipewa majukumu mbalimbali,
kama ifuatavyo:
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika
utozaji kodi, imeanzisha mfumo wa stempu za Kielektroniki ili kudhibiti
ujazo wakati wa uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki. Aidha,
Mamlaka itahakikisha kwamba wazalishaji na waingizaji nchini wa
malighafi ya pombe kali (ethanol) wamesajiliwa na kwamba mfumo wa
ufuatiliaji wa usambazaji malighafi hiyo unawekwa.
Wazalishaji
na waingizaji wa malighafi hiyo watawauzia wale tu ambao wamepewa
kibali na pia watatakiwa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu (3) ya
kiasi cha ujazo kilichouzwa na wateja waliouziwa ambao wamesajiliwa.
Uuzaji wa malighafi kwa watengezaji wa pombe kali ambao hawajasajiliwa
itakuwa ni kosa la jinai kulingana na Sheria.
Mkemia
Mkuu wa Serikali ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na
majumbani, atasajili makampuni na taasisi zinazoingiza kemikali za
viwandani na majumbani nchini ikiwa ni pamoja na Ethanol. Msajili
atawajibika kutoa taarifa sahihi za majina ya makampuni na watu binafsi
na taasisi zinazohusika, kiasi kilichoingizwa na kimetumika, pamoja na
madhumuni ya matumizi.
Kulingana
na sheria ya Leseni ya Vileo Na 28 ya Mwaka 1968 na marekebisho yake ya
mwaka 2012, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika
operesheni hii itaratibu zoezi hili katika mikoa, wilaya, tarafa, kata,
vijiji na mitaa yote Tanzania bara kwa kuhakikisha kuwa wanaofanya
biashara ya pombe ya kawaida na pombe kali (spirit) na watumiaji kinyume
na masharti ya leseni za vileo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo
vya sheria.
Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Viwango Tanzania
(TBS), katika operesheni hii watakukagua viwanda vyote vinavyojihusisha
na uzalishaji wa vileo na vifungashio vya aina mbalimbali vya kufungia
pombe kali kama vimekidhi viwango vya kitaifa Ukaguzi katika viwanda vya
plastiki utachunguza kama kuna mitambo ya kuzalisha vifungashio vya
plastiki kwa ajili ya pombe kali.
Mitambo
ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kama haitumiki kwa kuzalisha
bidhaa zingine katika kiwanda husika, mwenye kiwanda atalazimika kutoa
ufafanuzi wa hatima ya mitambo hiyo. Mitambo ya kuzalisha vifungashio
vya plastiki itakayokutwa inaendelea kuzalisha pombe kali na kufungashia
vifungashio vya plastiki itakamatwa na kutaifishwa na wahusika
watashtakiwa.
Wizara
ya Afya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee, kupitia Mamlaka ya Chakula
na Dawa (TFDA) na mabwana afya katika operesheni hii watatoa elimu kwa
umma na kukagua maeneo yote yanayotumika kuhifadhia, kuuza na kusambaza
vileo vya aina zote, na kushiriki kukamata vileo ambavyo vipo kinyume
cha sheria na kanuni.
Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari
Maelezo, itasaidia kutoa elimu kwa umma kuhusu suala hili.
Wizara
ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi, na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama, itashiriki katika operesheni, ikiwemo kwenye masuala
ya inteligensia.
Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, wataratibu operesheni.
Kama
tangazo letu la tarehe 20/2/2017 lilivyoonesha muda wa nyongeza unaweza
kutolewa kwa wazalishaji halali ambao wataonyesha ushahidi wa kuelekea
kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, na kwamba watahitaji muda mchache
kufanya hivyo, na ambao watatimiza masharti kadhaa na kupata kibali
maalum kabla ya tarehe 28/2/2017. Hadi sasa Serikali imepokea maombi ya
wazalishaji 9. Tutangaza kesho iwapo kuna ambao wamekidhi masharti au
la. Kanuni za upigaji marufuku pombe hizi zipo tayari.
Pia
tumepokea malalamiko kwa wazalishaji wengi kwamba zoezi hili limekuja
ghafla na wengine wana malighafi na bidhaa kwenye maghala. Ukweli ni
kwamba Serikali ilitoa taarifa Bungeni, kuanzia mwezi Mei 2016, na mara
kadhaa baada ya hapo, na rekodi zipo, kuhusu hatua hizi. Vilevile,
taarifa ya Serikali iliyotangaza kupiga marufuku pombe za viroba
ziliripotiwa kwa ukubwa stahiki kwenye vyombo vya habari, ikiwemo kwenye
ukurasa wa kwanza wa gazeti la Mwananchi, mwezi Agosti 2016. Katika
taarifa zote za nyuma, Serikali ilitangaza kwamba hatua hiyo itaanza
tarehe 1 Januari 2017. Hatua hizi zimechelewa kwa miezi miwili. Iwapo,
baada ya taarifa hizo za Serikali, kuna mzalishaji ameagiza malighafi au
kutengeneza au kuhifadhi pombe za viroba, au kuchukua mkopo kwa ajili
hiyo, atakuwa amefanya hivyo akijua madhara yake.
Mwisho
napenda kutoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika
utekelezaji wa zoezi hili la upigaji marufuku matumizi ya pombe
zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) kwa kutoa
taarifa kwa vyombo husika ili wale wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi
waweze kuchukuliwa hatua stahiki. Zawadi itatolewa kwa watakaotoa
taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watakaokiuka zuio hili.
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
28/02/2017
Post a Comment