Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha Hotuba ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 katika Kikao cha Bajeti cha
Baraza la Wawakilishi Zanzibar kilichoanza leo katika Majengo ya Baraza
hilo yaliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi
ya Manaibu Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
wakifuatilia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenye Baraza la Wawakilishi
Zanzibar.
Baadhi ya Manaibu Mawaziri wa
SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenye Baraza
la Wawakilishi Zanzibar.
Timu
ya Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ukiongozwa na
Katibu Mkuu wake Nd. Joseph Abdulla Meza wa Nne kutoka kulia wakiandika
dondoo wakati wa Hotuba ya Ofisi yao ikiwasilishwa na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar.
Mwakilishi
wa Jimbo la Tunguu Mh. Simai Mohamed Said wa kwanza kutoka Kulia na
Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake Mheshimiwa Suleiman Sarahan Said
wakiwa makini kufuatilia Hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar iliyowasilishwa Barazani.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuimarisha zaidi huduma za Kijamii
zikiwemo Elimu, Afya, Makaazi na upatikanaji wa Maji safi na salama
katika azma yake ya kutoa kipaumbele kwenye mpango wake wa maendeleo
katika kipindi cha mwaka 2017/2018.
Mpango
huo utakwenda sambamba na uimarishaji wa Miundombinu ya uingiaji Nchini
inayojumuisha Bandari, Viwanja vya Ndege , bara bara za ndani , Nishati
pamoja na Tafiti zitakazosaidia kutoa maamuzi katika mipango hiyo ya
Maendeleo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati
akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Kikao cha Bajeti cha Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kilichoanza leo katika Majengo ya Baraza hilo
yaliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi
Seif alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kugharamia
uendeshaji wake na kutoa huduma bora kwa Wananchi kwa kutumia rasilmali
zilizopo kwa umakini mkubwa na kuhakikisha matumizi yote yanaleta tija
kwa Umma.
Alisema
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020 ikiwa katika kipindi cha
mwisho cha miaka mitano unaenda sambamba na uidhinishwaji wa awamu ya
Tatu ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini { MKUZA 111}.
Balozi
Seif alieleza kwamba hiyo inamaanisha wazi kwamba Malengo ya Taifa bado
yanadhamiria utekelezaji wa Mipango hiyo Mikuu ambayo imekusudia kukuza
Uchumi, kuimarisha huduma za Jamii pamoja na kuimarisha Demokrasia na
Utawala Bora.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba hali ya ukuaji
wa uchumi wa Nchi imepelekea kuongezeka kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2016
ambalo limeongezeka na kufikia thamani ya Shilingi 2,309.5 Bilioni
ikilinganishwa na thamani ya shilingi 1,633.0 Bilioni Mwaka 2015.
Alisema uchumi wa Zanzibar umeimarika kwa asilimia 6.8 mwaka 2016
kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015 hali iliyo tofauti na taswira
inayojionyesha kwa mwenendo wa ukuaji wa Uchumi kwa Nchi za Kusini mwa
Jangwa na Sahara ambapo kasi ya ukuaji wa uchumi imeshuka na kufikia
wastani wa asilimia 1.6 mwaka 2016 kutoka wastani wa asilimia 3.4 mwaka
2015.
Akigusia mvua za masika zinazoendelea kunyesha hapa Nchini na
kuleta athari kubwa kwa Wananchi walio wengi Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif aliwatahadharisha Wananchi kuendelea kuchukua
tahadhari za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo miripuko
ya maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa maji.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inawasisitiza
Wananchi kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi ambayo mazingira yake
yanaweza kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa hasa wakati wa mvua
kubwa zinazonyesha kama mabondeni, kwenye njia za asili za maji na
pembezoni mwa milima hasa Kisiwani Pemba.
Balozi Seif alitoa wito kwa wananchi kuendelea kufuata maelekezo
yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya usafi wa mazingira ikiwemo
kunawa mikono mara watokapo kujisaidia na kabla ya kula.
Kwa upande wa wafanyabiashara Balozi Seif aliwakumbusha kuendelea
kufuata masharti yaliyowekwa juu ya biashara zao kwa kuzingatia suala la
usafi na ulinzi wa afya za Wananchi ili kujikinga na maradhi ya
mripuko.
Akigusia janga a dawa za kulevya linaloendelea kuiathiri jamii
Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali
yaMapinduzi ya Zanzibar kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti
wa Dawa za Kulevya imetoa mafunzo kwa wadau katika shehia zenye Banadari
Rasmi na zisizo Rasmi.
Alisema hatua hiyo ililenga kuweka wazi mbinu mbali mbali
zinazotumiwa na wahalifu katika kupitishia dawa za kulevya ambapo
washiriki wa mafunzo hayo wapatao 186 walitoa kwenye Shehia zipatazo 94
zenye Bandari hizo.
Balozi Seif alisema Kamati ya Kitaalamu ya Tume hiyo iliweza
kupanga mikakati ya udhibiti wa dawa za kulevya, uimarishaji wa kinga
dhidi ya matumizi ya dawa hizo pamoja na kuzisaidia Nyumba za upataji
nafuu kwa vijana walioathirika na dawa za kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Nchi Rafiki,
Taasisi, Makampuni na washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi
waliojitolea kuunga mkono harakati za Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar
na kupiga hatua kubwa Kiuchumi na ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema michango ya washirika na Mataifa hayo marafiki
imewezesha kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa huduma
bora za Kijamii na kuleta maendeleo katika Taifa zima.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliliomba Baraza la Wawakilishi
liidhinishe jumla ya shilingi Bilioni 44,837,577,000/- kwa Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Taasisi zake kwa ajili ya
kutekeleza Programu zake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
10/5/2017.
Post a Comment