Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI
ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara nyingine tena
imefanya upimaji wa moyo wa mtoto aliye tumboni mwa mama yake,
kuchunguza magonjwa mbalimbali ya moyo.
Upimaji huo umefanywa katika taasisi hiyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI, Naiz Majani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Naiz amesema kuna faida lukuki iwapo mjamzito ataamua kufanya kipimo maalumu.
"Tunatumia
Ultra sound kama kawaida kufanya kipimo hiki, lakini inakuwa ina
tofauti kidogo... hatutumii mionzi yoyote, hivyo hakuna madhara
anayoweza kuyapata mama au mtoto wake aliye tumboni," amesema.
Ametaja
faida hizo kuwa ni kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa na
magonjwa ya moyo, na kuwaondoa kwenye masumbufu wanayoweza kuyapata
kutokana na kuchelewa kupata matibabu.
"Kwa
mara ya kwanza tuliwafanyia kipimo hicho wajawazito 25 mwishoni mwa
mwaka jana ambapo watano kati yao mimba zao zilikutwa na matatizo.
"Wajawazito
hao wanatarajiwa kujifungua wakati wowote kuanzia sasa na watoto hao
wataanza kufuatiliwa kwa ukaribu na kupewa matibabu ya haraka," amesema.
Amesema
waliamua kuanza kufanya kipimo hicho baada ya kugundua watoto kadhaa
hufikishwa katika taasisi hiyo wakiwa katika hatua mbaya kiasi cha wao
kushindwa kuwapatia matibabu.
Amesema inakadiriwa katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini mmoja anakuwa amezaliwa na magonjwa ya moyo.
"Mwaka
jana inakadiriwa walizaliwa watoto milioni moja, kwa msingi huo watoto
wapatao 12,000 walizaliwa na magonjwa haya lakini tuliowaona kliniki
yetu ni kati ya 700 hadi 750 pekee," amesema.
"Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo yanatakiwa kutibiwa mapema, lakini wanakuja umri umeshakwenda tunashindwa kuwasaidia," amesema.
Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema dhumuni kubwa la kuanzisha huduma hiyo ni kugundua matatizo hayo mapema.
"Tunahamasisha kina mama wajitokeze, Tanzania sasa imepiga hatua kubwa,
tunafanya hivi kwa sababu asilimia 85 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji
ni watoto.
"Na hawa ndiyo tunaowategemea kuwa Taifa la kesho, tusipowagundua na
kuwatibu mapema maana yake ni kwamba watakuja kuwa mzigo kwa Taifa miaka
ijayo," amesema.
Amefafanua
kwamba miaka ya nyuma si kwamba magonjwa ya moyo hayakuwapata watoto
bali hayakuweza kugundulika kutokana na uhaba wa wataalamu, vifaa.
"Watoto
wengi walikufa kwa kile kilichoelezwa ama ni typhoid, nimonia au surua,
leo hii wataalamu tupo, tulikwenda kujifunza kwa wenzetu katika nchi
zilizoendelea ili tuisaidie nchi yetu, magonjwa yote ya moyo
yanatibika," amesisitiza.
Post a Comment