Rais Magufuli aamuru madaktari 258 walioomba kufanya kazi nchini Kenya waajiriwe nchini mara 1
Mnamo tarehe 18 Machi 2017 Ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dkt. Cleopa Mailu uliwasili nchini ambapo ulikutana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dhumuni la mkutano huo ulikua kuomba kuajiri, kwa Mkataba, Madaktari wa Tanzania mia tano (500), ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya.
Mheshimiwa Rais JPM, alikubali ombi hilo.
Mnamo tarehe 18 Machi, 2017, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitangaza nafasi hizo za ajira kwa Madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Maombi hayo yalipokelewa ambapo hadi tarehe 27 Machi, 2017 jumla ya maombi 496 yaliwasilishwa. Baada ya kufanya uchambuzi wa maombi haya ilibainika kuwa, Madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Baadhi ya vigezo hivyo ni pamoja na:
1.Uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya Sekondari.
2.Chuo alichosoma na mwaka wa kuhitimu masomo.
3.Sehemu alikofanya mafunzo ya vitendo (Intership) na mwaka wa kuhitimu mafunzo hayo.
4.Uzoefu wa kazi.
5.Umri wa mwombaji usizidi miaka 55.
6.Usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari la Tanganyika.
7.Asiwe mtumishi wa Umma, Hospitali Teule za Halmashauri na Hospitali za Mashirika ya hiyari wanaolipwa mishahara na Serikali.
Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari wake kufanya kazi nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na kuandaa Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo za Madaktari na Mikataba wa Ajira kwa Madaktari hao, wananchi (Madaktari) watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi Mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri Madaktari kutoka Tanzania.
Kwa kuwa ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za Madaktari ilikubalika na pande zote mbili kuwa iwe imekamilika ifikapo tarehe 6 Aprili, 2017 na kwamba Madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili, 2017 na kwa kuwa hadi tarehe ya taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za Madaktari wa Tanzania nchini Kenya, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua kuwa, Madaktari hao 258 ambao waliokuwa tayari kwenda kufanya kazi nchini Kenya waajiriwe na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara moja.
Kufuatia uamuzi huu, Majina ya Madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya Wizara www.ehealth.go.tz.
Aidha, Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kupeleka Madaktari wetu nchini Kenya.
Imetolewa na:
Ummy A. Mwalimu (Mb),
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto,
Chuo Kikuu cha DODOMA,
S.L.P. 743,
DODOMA.
19 Aprili, 2017
Post a Comment