Yahya Jammeh afungasha virago na kutimkia Equatorial Guinea
Aliyekuwa Rais wa muda mrefu wa Gambia, Yahya Jammeh ameondoka nchini humo Jumamosi usiku na kwenda nchini Equatorial Guinea baada ya kushindwa uchaguzi na kugomea kuondoka madarakani hali ambayo ilizifanya nchi za jirani kutumia diplomasia kumuondoa madarakani.
Jammeh amedaiwa kuondoka na mali za mamilioni ya pesa pamoja na magari ya kifahari.
Kuondoka kwake kumehitimisha na utawala wake wa miaka 22 wa kidikteta na migogoro ya kisiasa ambayo ilipelekea nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufikia katika hali ya majeshi ya kieneo kuingia kwa nguvu kumuondosha mtawala huyo madarakani.
Jammeh hakutoa tamko lolote wakati anaondoka kwenye uwanja wa ndege wa Banjul na familia yake katika ndege iliyokuwa haina alama yoyote, na kwenda nchini Equatorial Guinea.
Alikuwa amefuatana na Rais wa Guinea, Alpha Conde, ambaye alipendekeza awe msimamizi wa kutafuta ufumbuzi juu ya njia ya kumuondosha nchini kwa kuzungumza naye.
Kuondoka kwake Jammeh, ambaye alichukuwa madaraka kwa njia ya mapinduzi mwaka 1994, kumemaliza wiki kadhaa za mvutano zilizoanza mara alipokataa kuachia madaraka kufuatia ushindi aliopata mpinzani wake katika uchaguzi wa mwezi Desemba 1.
Pia kuondoka kwake kumeepusha uingiliaji kati wa jeshi lenye askari 7000 kutoka Senegal na Nigeria ambao tayari walikuwepo nchini Gambia Alhamisi ili kukabiliana na wafuasi wa Jammeh katika jeshi lake.
Kuondoka kwake kumefungua njia kwa Adama Barrow kuchukua madaraka, ambaye alishinda uchaguzi wiki saba zilizopita.
Barrow ambaye aliapishwa Alhamisi kwenye ubalozi wa Gambia nchini Senegal, hivi sasa anatarajiwa kurejea nyumbani.
Post a Comment