TFF watoa taarifa kuhusu mchezaji Venance Ludovick
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewataka wadau wa mpira wa miguu nchini wapuuze taarifa za kwenye mitandao kuhusu mchezaji Venance Ludovick.
Suala la mchezaji huyo linaendelea kufanyiwa kazi na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji. Tunawahakikishia umma wa wapenda soka nchini kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa kanuni zinazoendesha mashindano husika.
Mchezaji huyo analalamikiwa na timu ya Yanga kwa kucheza katika mechi yao dhidi ya African Lyon iliyochezwa Desemba 23, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kufungana bao 1-1, huku kwa Lyon bao lao likifungwa na mchezaji huyo.
Hata hivyo, mara baada ya mechi hiyo, timu ya Yanga ilikata rufaa katika Kamati hiyo ikitaka timu hiyo ipokwe ushindi kutokana na kumchezesha mchezaji huyo, ikidai kuwa hakukamilisha taratibu za usajili kutoka katika timu ya Mbao FC ya Mwanza na kwamba bado alikuwa na mkataba wa kuichezea timu hiyo.
Post a Comment