RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, YA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2017
Assalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh
Ndugu Wananchi,
Tuna
wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muweza wa kila
jambo kwa kuturuzuku neema ya uhai tukaweza kuifikia siku hii tunapouaga
mwaka 2016 Miladiya na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017. Hapana shaka,
kwamba tuliuanza mwaka 2016 tukiwa na wenzetu ambao kwa mapenzi ya
Mwenyezi Mungu, wameshatangulia mbele ya haki. Tumuombe Mola wetu awape
malazi mema peponi na sisi tulio hai atujaalie kila la kheri katika
maisha yetu hapa duniani na atupe hatma njema. Amin!
Ndugu Wananchi,
Tunamshukuru
Mwenyezi Mungu; Subhana Wataala kwa kutuwezesha kuyakabili kwa
mafanikio makubwa masuala mbali mbali tuliyoyatekeleza katika mwaka
2016, ambao sasa tunaouaga. Mtakumbuka kwamba miongoni mwa matukio
makubwa ya mwaka 2016, ni kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25
Oktoba, 2015 ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar pamoja na
matokeo yake. Uchaguzi huu ukarudiwa tena tarehe 20 Machi, 2016.
Katika uchaguzi huo wananchi walishiriki kupiga kura kwa amani na
kuitumia vyema haki ya kidemokrasia na kikatiba ya kuwachagua viongozi
wanaowataka. Kwa mara nyengine wananchi mlionesha imani yenu kwa Chama
cha Mapinduzi na mimi mkanichagua kwa asilimia 91.4 na vile vile,
mmewachagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM. Uamuzi wenu huo
mmeiwezesha CCM kuunda Serikali, pamoja na kupata idadi kubwa ya Wajumbe
wa Baraza la Tisa la Wawakilishi na Baraza hilo nililizindua tarehe 05
Aprili, 2016. Kwa niaba ya viongozi wenzangu wote kwa mara nyengine
tunatoa shukurani zetu kwenu na kuahidi kukutumikieni kwa uwezo wetu
wote.
Ndugu Wananchi,
Katika
kipindi kisichozidi mwaka mmoja, wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar Awamu ya Saba, kwenye kipindi hiki cha pili, nchi yetu imepata
mafanikio ya kuridhisha katika utekelezaji wa mipango yetu mikuu ya
maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020, MKUZA, Ilani ya
Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 pamoja na mipango mingine ya
kisekta. Tathmini tuliyoifanya hadi tunapouaga mwaka 2016 na
kuukaribisha mwaka mpya wa 2017, inaonesha tumeweza kupiga hatua katika
malengo yetu ya kuinua uchumi na kuimarisha huduma za jamii, zikiwemo
afya, elimu na huduma za maji safi na salama na nyenginezo.
Ndugu Wananchi,
Uchumi
wetu umeendelea kuimarika. Kwa mwaka 2015, Pato Halisi la Taifa
lilikua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.6. Hadi kufikia robo
mwaka ya pili (Aprili - Juni) mwaka 2016 uchumi umekua kwa kasi ya
asilimia 6.2. Kadhalika, tumefanikiwa kuongeza kiwango cha kukusanya
kodi. Kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, 2016 Serikali imeweza
kukusanya jumla ya TZS bilioni 441.3 kutokana na vyanzo vyetu vya ndani.
Kwa kipindi kama hicho mwaka jana (2015) tulimudu kukusanya TZS bilioni
336.6. Hii ina maana kwamba kwa miezi kumi ya mwanzo ya mwaka 2016,
mapato yetu yameongezeka kwa TZS bilioni 104.7 sawa na ukuaji wa
asilimia 31.1. Sambamba na mafanikio hayo, washirika wetu wa maendeleo
wameithamini sana kazi nzuri tunayoifanya ya kuwaletea maendeleo
wananchi. Katika kuthibitisha imani yao kwetu, Serikali imepokea jumla
ya TZS bilioni 54.53 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kati ya mwezi wa
Januari hadi Oktoba, 2016. Kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 tulipokea
TZS bilioni 47.47, sawa na ongezeko la asilimia 14.9. Huu ndio ukweli
halisi na hio ndiyo hali halisi ambayo ni vyema wananchi mkaifahamu
kuwa ni nzuri; kinyume na maelezo yanayotolewa na baadhi ya watu ambao
hawana taarifa sahihi na takwimu za uhakika za Serikali yetu.
Tutajidhatiti zaidi katika mwaka ujao na Mwenyezi Mungu akipenda mambo
yatakuwa bora zaidi.
Ndugu Wananchi,
Kwa
upande wa huduma za jamii mwaka unaomalizika, utakumbukwa kwa hatua za
mafanikio tuliyoyapata katika kuimarisha huduma za afya nchini. Tarehe
11 Novemba, 2016 tulizindua majengo ya wodi mpya ya watoto na wodi ya
wazazi katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja. Wodi hizo zimetiwa vifaa
vya kisasa vya kutolea huduma, na kuwa na nafasi ya kutosha kwa wagonjwa
watakaofika kuhudumiwa. Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa
lengo la Serikali la kuifanya Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya
rufaa kamili na kuimarishwa kwa huduma zake.
Kadhalika,
tarehe 26 Novemba, 2016 tulifanya uzinduzi mwengine nao ni wa Hospitali
ya Abdalla Mzee, Mkoani Pemba baada ya kujengwa upya kwa msaada wa
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Kufunguliwa kwa hospitali ya
Abdalla Mzee ambayo sasa imefikia hadhi ya Hospitali ya Mkoa
kutawawezesha wananchi wa Pemba kupata huduma mbali mbali za afya ambazo
mwanzoni walilazimika kuzifuata nje ya Kisiwa cha Pemba. Dhamira ya
Serikali ni kuyaendeleza mafanikio hayo katika mwaka ujao, kwa kuzidi
kuchukua hatua ili huduma za afya nchini ziimarike zaidi na ziwe za
viwango bora. Maelekezo ya kina ya mafanikio tuliyoyapata kwa kila
sekta, penye majaaliwa nitayatoa katika hotuba yangu ya kilele cha
maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ifikapo tarehe
12 Januari, 2017.
Ndugu Wananchi,
Kwa
lengo la kuwaenzi wazee wetu na kuthamini mchango wao katika maendeleo
ya nchi yetu, Serikali, katika mwaka unaomalizika, ilianza utekelezaji
wa Mpango wa Pencheni ya Jamii. Kupitia mpango huu wazee wote
waliofikia umri wa miaka 70 na kuendelea waliosajiliwa, wameanza kupewa
posho la TZS 20,000 kwa mwezi. Kuanzia mwezi Aprili 2016, tulipoanza
utaratibu huu, idadi yao imeongezeka kutoka watu 21,263 waliosajiliwa
mwaka 2015, hadi kufikia watu 26,603 mwezi wa Novemba, 2016.
Hivi
sasa Serikali inaendelea kuwasajili watu wengine waliotimiza sifa za
kuwemo katika mpango huo ambao hapo mwanzo hawakusajiliwa. Vile vile
tutazifanyia kazi changamoto zilizojitokeza kwa lengo la kuongeza
ufanisi katika utekelezaji wa mpango huo. Kadhalika, Serikali
inazingatia haja ya uwezekano wa kuongeza idadi ya wazee wanaopaswa
kuwemo kwenye mpango huu, kwa kupunguza umri hadi kufikia miaka 65
badala ya miaka 70 kama ilivyo hivi sasa. Vile vile, tunazingatia haja
ya kuwaandalia wazee huduma za afya kwa dhamira ile ile ya kuwatunza na
kuwaenzi wazee wetu.
Ndugu Wananchi,
Tukio
jengine mahususi katika mwaka tunaoumaliza lilikuwa ni kutiwa saini kwa
Sheria Namba 6 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya
mwaka 2016 inayoipa Zanzibar uwezo wa kisheria wa kushughulikia
utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Hili ni tukio kubwa,
ambalo kwa umuhimu wake tuliamua kulifanya hadharani hapo tarehe 15
Novemba, 2016, kwenye ukumbi wa Ikulu, mbele ya viongozi mbali mbali,
wafanyakazi, wananchi na wafanyakazi wa vyombo vya habari. Kufuatia
hatua hii, Zanzibar imepata uwezo wa kisheria wa kushughulikia utafutaji
na uchimbaji wa rasilimali hizi muhimu ili nazo ziweze kuchangia pato
la uchumi wetu. Hadi sasa mipango yetu katika suala hili inaendelea
vizuri. Tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya wawekezaji wenye uwezo
mkubwa na uzoefu wa masuala ya mafuta na gesi asilia ambao wana nia ya
kuwekeza nchini kwetu.
Ndugu Wananchi,
Katika
mwaka tunaoumaliza, Serikali iliendelea kufanya jitihada katika
kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini kama ilivyo kwa mataifa
mengine duniani. Katika jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi
kupitia Mfuko wa Uwezeshaji kwa kutoa mikopo kwa wananchi
wanaojishughulisha na biashara, kilimo, uvuvi, ufugaji na nyenginezo,
vile vile, Serikali iliandaa Kongamano na maonesho ya Wajasiriamali
tarehe 03 Disemba, 2016 na tarehe 04 Disemba, 2016 ambapo maonyesho hayo
yalifanyika katika jengo la zamani la Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.
Lengo
la kongamano na maonesho hayo lilikuwa ni kutoa fursa kwa wajasiriamali
kujifunza mbinu bora za kufanya shughuli zao ili kuongeza tija. Aidha,
shughuli hiyo ilikuwa na lengo la kuongeza hamasa na taaluma, hasa kwa
vijana ili waweze kuzifahamu fursa ziliopo katika ujasiriamali, kwa
lengo la kujiajiri wenyewe na kuondokana na hisia za kutegemea ajira
chache zinazopatikana Serikalini. Katika mwaka ujao, Serikali
itaendeleza jitihada za kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwapatia fursa
zaidi za mikopo, kutafuta masoko ya bidhaa zao na kuwapa mafunzo kwa
njia ya mafunzo mbali mbali, zikiwemo semina na makongamano pamoja na
kukiendeleza kituo cha kukuza na kulelea Wajasiriamali, kilichopo
Mbweni.
Ndugu Wananchi,
Katika
kuimarisha Maadili ya Viongozi na utawala bora, Serikali katika mwaka
2016 ilikamilisha uundaji wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo
tayari imeshaanza kufanya kazi zake. Madhumuni ya kuchukua hatua hizo
ni katika utekelezaji wa matakwa ya kisheria kwa mujibu wa sheria ya
Maadili Namba 4 ya mwaka 2015. Miongoni mwa majukumu ya Tume ya Maadili
ni kuhakikisha kwamba viongozi wa umma na wale wote waliotajwa katika
sheria ya Maadili, wanajaza fomu ya tamko la rasilimali na madeni ambazo
tayari zimekwishatolewa kwa wahusika na kutakiwa kuzirejesha Tume fomu
hizo, si zaidi ya tarehe 31 Disemba, 2016.
Napenda
nisisitize kauli yangu niliyoitoa tarehe 10 Disemba, 2016 katika
maadhimisho ya siku ya Maadili kwenye viwanja vya bustani ya Victoria,
ya kuwataka wanaohusika wote wazingatie maelekezo yaliyotolewa kwenye
fomu hio na waepuke kutoa taarifa zisizo za kweli, kwani kufanya hivyo
ni kitendo cha kuvunja maadili ya uongozi. Aidha, nahimiza kuwa kila
mmoja wetu azingatie kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya maadili
isemeyo:“Imarisha utawala bora kwa kukuza uadilifu, uwajibikaji, haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa.” Huo
ni ujumbe muhimu wa kuuzingatia wakati tunapouanza mwaka mpya wa 2017.
Sote tuazimie kuitekeleza kauli hii kwa vitendo, kwani nchi yetu
inaongozwa kwa kufuata sheria na misingi hiyo muhimu ya utawala bora.
Ndugu Wananchi,
Katika
kusherehekea kumalizika kwa mwaka huu na kuja kwa mwaka mpya, wapo
baadhi ya watu ambao husherehekea kwa vitendo ambavyo huweza kuharibu
amani na utulivu na kusababisha usumbufu kwa watu wengine. Ni vyema
sote tuzingatie umuhimu wa kuitunza amani, umoja na mshikamano wetu
kwani ndiyo msingi wa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika nyanja za
uchumi, siasa na ustawi wa jamii. Kwa hivyo, kila mmoja wetu ana jukumu
la kudumisha amani kwani Serikali haitosita kumchukulia hatua mtu
yeyote au kikundi chochote kitakachofanya vitendo vinavyohatarisha amani
na usalama wa wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea nchi
yetu.
Ndugu Wananchi,
Wakati
tunauaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017, nchi yetu bado
inakabiliwa na changamoto mbali mbali, zikiwemo athari za mabadiliko ya
tabianchi, zinazoathiri ufanisi katika utekelezaji wa mipango yetu ya
kiuchumi na maendeleo. Tuna changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa
vijana na tatizo la kuendelea kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji wa
wanawake na watoto. Taarifa kutoka katika Jeshi la Polisi Zanzibar
zinaonesha kuwa idadi ya makosa ya udhalilishaji wa kijinsia,
yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi, yameongezeka kutoka makosa 169
mwaka 2015 hadi kufikia makosa 512, kati ya Januari hadi wiki ya pili
ya Disemba, 2016 sawa na ongezeko la asilimia 203. Hii si taarifa
nzuri. Natoa wito kwa wananchi wote tushirikiane katika kuvikomesha
vitendo vya udhalilishaji. Ni dhahiri kuwa ufumbuzi wa changamoto hizi
unahitaji mchango wa kila mmoja wetu na sio Serikali peke yake.
Sote
tuna wajibu wa kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango
yetu ya maendeleo pamoja na kutii sheria bila ya kushurutishwa.
Mafanikio yetu ya sasa na yale ya baadae yanategemea sana ushirikiano na
umoja wetu, katika kujenga nchi yetu. Mambo hayo muhimu yawe ndiyo
dira yetu. Ni jukumu letu sote kwa pamoja na lazima tutimize wajibu
wetu huo.
Ndugu Wananchi,
Kwa
kumalizia risala yangu hii, napenda nikukumbusheni kwamba tarehe 12
Januari, 2017, tunaadhimisha Miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar. Sote tuna wajibu wa kuyasherehekea na kuyadumisha Mapinduzi
kwani ndiyo yaliyotukomboa. Wito wangu kwenu ni kwamba kila mmoja wetu
ajitahidi kushiriki katika maadhimisho yetu hayo yanayotanguliwa na
shamra shamra mbali mbali za uzinduzi wa miradi ya maendeleo kwa uwekaji
wa mawe ya msingi. Aidha, jambo hili litaongeza chachu ya sherehe zetu
tutakaposhiriki katika siku ya kilele kwenye Uwanja wa Amaan ili
kuzifanikisha sherehe hizi adhimu na muhimu.
Namalizia
risala yangu kwa kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa
Zanzibar, Tanzania Bara, ndugu na marafiki wote popote walipo.
Kadhalika, natoa salamu kwa viongozi wa nchi marafiki, Taasisi za
kimataifa na washirika wetu mbali mbali wa maendeleo. Mola wetu
aujalie kheri na baraka nyingi mwaka mpya wa 2017. Aiongezee nchi yetu
amani, umoja, mshikamano na mapenzi baina yetu. Mwenyezi Mungu atupe
uwezo wa kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Post a Comment