KILICHOMPONZA KIGOGO WA TANESCO KUTUMBULIWA
HATUA ya Shirika la Umeme ya kupandisha bei ya umeme bila kushirikisha
mamlaka nyingine za Serikali, zimemgharimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika
hilo Felchesmi Mramba, ambaye jana amefutwa kazi na Rais John Magufuli.
Kabla ya kutengua uteuzi wa Mramba, Rais Magufuli ambaye jana alisali
mjini Bukoba katika kanisa la Bikira Maria, Mama mwenye Huruma la mjini
Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye, Makamu wa Rais, Waziri
Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo.
Ewura juzi ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 baada ya
Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia 18.19, lakini hatua hiyo
ilisitishwa na Profesa Muhongo.
“Waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi,
hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana, ya nishati hawakumuuliza hata
Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu akae pekee yake na afanye
maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka nyingine,” alisema Rais.
Ateua bosi mpya
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson
Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya kutengua uteuzi wa Mramba,
amemteua Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Mwinuka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na hadi uteuzi
wa jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda
Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiwa kanisani, Rais Magufuli alimpongeza Profesa Muhongo kwa hatua ya kusimamisha kupanda kwa bei ya umeme.
“Namshukuru waziri wa nishati kwamba ameshatengua maamuzi hayo, kwa hiyo
umeme hakuna kupanda.” Rais Magufuli alisema haiwezekani watu mnapanga
mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika mikakati hii mikubwa ya nchi
ya kusambaza umeme hadi vijijini na umeme huo unaenda hadi kwa watu
maskini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee kwa sababu ya
cheo chake anakwenda kusimama kupandisha bei ya umeme.
Akionekana kukereka kwa hatua hiyo ya kupandishwa kwa bei ya umeme, Rais
Magufuli alisema, “Na ndio maana baba askofu nalizungumza hili kwamba
majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua, ndio maana naomba sana
Watanzania muendelee kutuombea, lengo la serikali ninayoiongoza ni
kwenda na wananchi wa kipato cha chini.”
Prof Muhongo alivyoikaanga Tanesco Juzi usiku
Profesa Muhongo alimwandikia barua Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi ya kumtaka kusitisha ongezeko
la bei ya umeme iliyokuwa ianze kutumika jana. Profesa Muhongo alitoa
uamuzi huo chini ya sheria ya umeme ya mwaka 2008 ambayo inampa mamlaka
waziri mwenye dhamana ya nishati.
“Leo Desemba 31, 3016 Ewura inaamuliwa kusitisha utekelezaji wa bei mpya
za umeme uliyotangaza jana hadi hapo Serikali itakapopitia ripoti ya
Ewura.”
Akizungumza na kituo kimoja cha radio jana, Profesa Muhongo alisema
alisitisha uamuzi wa Ewura kwa sababu taratibu hazijafuatwa. Alisema pia
Watanzania wote waliohojiwa walipinga ombi la Tanesco la kupandisha
umeme.
“Ewura walitumia kigezo gani cha kuongeza bei, kama walitumia kigezo
ambacho wengi hatukijui basi huo ni uamuzi wao wenyewe,” alisema.
Alisema taratibu zilizopo ni kwamba mara Tanesco wanapoomba kupandisha
bei za umeme na Ewura ikishasikiliza maoni ya wadau, kabla ya kutangaza
uamuzi ni lazima waziri mwenye dhamana na nishati ajulishwe kwanza.
“Lakini hivi ninavyozungumza na wewe hata mimi nilishtushwa jana
naambiwa Ewura wametangaza, mimi nilikuwa sijapata chochote kutoka
Ewura, mimi sijajadiliana na Ewura wala sijajadiliana na Tanesco
kutokana na zoezi zima la kutaka kuongeza bei,” alisema.
Alisema waziri hashirikishwi ila anatakiwa kupokea taarifa ya mwisho,
“hadi leo nimesikia tu, sijapokea hiyo taarifa, nenda kawaulize Ewura na
Tanesco kama nina ripoti yao ya mwisho.
Alisema matatizo ya Tanesco hayatatuliwi kwa kuongeza bei, alisema
matatizo ya shirika yanatokana na uongozi wa Tanesco na mambo mengine
ambayo yanafahamika.
Alisema Ewura lazima ipeleke mapendekezo yake Wizara ya Nishati na
Madini. Profesa Muhongo alisema hapo ndipo waziri atawaita Ewura na
Tanesco kujadiliana na wakikubaliana hapo ndipo wataenda kutangaza hiyo
bei.
Alisema haiwezekani Ewura ni chombo cha Serikali hivyo haiwezi kufanya bila waziri kufahamu.
Alisema tatizo la madeni ya Tanesco sio kuongeza bei ya umeme, alisema
Serikali kwa sasa imefuta fedha za mikopo ya nje kwa ajili ya kulipa
deni la Tanesco, hatuwezi kutafuta fedha za kulipa deni za kulipa madeni
hayo kwa Watanzania halafu shukrani iwe ni kuongezewa bei ya umeme.”
Alisisitiza kuwa matumizi ya fedha ya Tanesco ni mabaya kwa sababu kila
mwisho wa mwaka viongozi peke yake wanalipana bonus na akatoa mfano wa
mwaka jana alifuta maamuzi hayo wakati tayari viongozi wameshapitisha
uamuzi wa kulipana kati ya Sh milioni 60 na Sh milioni 40.
“Hivi kweli Tanesco wanafanya kazi nzuri, wanatuongezea bei ili walipane posho?” aliuliza.
Ahadi ya wizara kwa umma Waziri Muhongo akiwasilisha Hotuba ya Makadirio
ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2016/17 ya wizara hiyo bungeni mjini
Dodoma mwaka jana kuhusu upatikanaji wa huduma ya umeme nchini, alisema
kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme (access level), kimekuwa
kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Watanzania waliofikiwa na huduma hiyo, ameongezeka kutoka asilimia 36
mwezi Machi 2015 hadi kufikia takriban asilimia 40 mwezi Aprili, 2016.
Alisema ongezeko hilo limetokana na juhudi za Serikali za kusambaza
umeme nchini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO).
Kuhusu punguzo la viwango vya bei za umeme, Profesa Muhongo alisema
Serikali imetekeleza ahadi yake ya kupunguza bei za umeme kuanzia Aprili
Mosi mwaka 2016 kwa kati ya asilimia 1.5 na 2.4.
Alisema Serikali pia imeondoa tozo ya kuwasilisha maombi ya
kuunganishiwa umeme (application fees) ya Sh 5,000 na tozo ya huduma ya
mwezi (service charge) ya Sh 5,520 kwa Wateja wa Umeme kwa Daraja la T1
na D1, ambao wengi wao ni wa majumbani.
Hatua hii itawasaidia watumiaji wadogo wa umeme mijini na vijijini
kumudu gharama hizo, hivyo kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi
Ewura ilivyobariki ongezeko Juzi Ewura ilitangaza kupandisha bei ya
umeme kwa asilimia 8.5 badala ya asilimia 18.19 iliyokuwa imeombwa na
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco).
Bei hizo mpya ilikuwa zianze kutumika jana Januari mosi, 2017.
Akitangaza ongezeko hilo la bei, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura alisema,
mamlaka yake imefikia uamuzi wa kuongeza asilimia 8.5 kutokana na
kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wake.
Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) ambalo linanunua umeme wa jumla
kupeleka Zanzibar limeongezewa kwa asilimia 5.7 ya bei ya umeme.
Ongezeko hilo halikuwahusu wateja wa majumbani ambao matumizi yao
hayazidi uniti 75 kwa mwezi ambao wengi ni wananchi wa vijijini ambao
wanatumia umeme kwa kuwasha taa tu.
Sababu kupandisha umeme
Oktoba mwaka huu Tanesco iliomba kupandisha bei za umeme kwa maelezo
kuwa gharama za uendeshaji katika uzalishaji na usafirishaji wa umeme
zilikuwa juu hivyo kuna haja ya kupandisha bei za umeme.
Hatua hiyo ilikuja ikiwa ni miezi saba tangu kutangazwa kwa bei mpya ya
umeme iliyokuwa na punguzo la asilimia 1.5 hadi 2.4 sanjari na kuondoa
tozo ya kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na gharama ya huduma kwa kila
mwezi ambayo ilikuwa na Sh 5,520.
Wakati inaomba kupandisha bei aliyekuwa mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi
Mramba alisema ombi la mabadiliko ya bei za umeme ambalo
waliliwasilisha Ewura Oktoba mwaka jana ni kutokana na agizo la
kubadilisha bei za umeme la mwaka 2016 lililoanza kutumika Aprili 2016.
Alisema ifahamike kuwa bei za umeme zilitolewa zilitakiwa zitumike mpaka
31/12/2016, hivyo itakapofika Januari 2017 inatakiwa bei mpya za umeme
kutolewa kwa mujibu wa sheria.
“Hivyo Taneso ilitakiwa kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji umeme na kupeleka mapendekezo hayo kwenye
Ewura ili kupitiwa na kufanyiwa taftishi, kupata maoni ya wadau ikiwa ni
pamoja na baraza la ushauri la Serikali."
Hivyo basi ikiwa bei za umeme zitapanda au kutopanda, hiyo itategemea na
mapitio ya tathmini ya gharama za kuzalisha, kusafirisha na kusambaza
umeme tulizowasilisha Ewura.
Alisema Tanesco haiwezi kuamua yenyewe kupandisha au kutopandisha bei za umeme.
Aliongeza kuwa kupanda au kushuka kwa gharama za umeme ni suala la
kisheria na ni jambo la kawaida kwani bei ya umeme imeshawahi kushuka
katika vipindi tofauti.
Mramba alitoa mfano mwaka 2015 robo ya kwanza ya mwaka bei ilishuka kwa
asilimia 2.5 na vivyo hivyo Aprili mwaka 2016 pia gharama za umeme
zilishuka kwa asilimia 1.6.
Askofu Kilaini asifia Katika mahubiri yaliyoendeshwa na Askofu Msaidizi
wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alipongeza jitihada za
Rais Magufuli hasa kuhakikisha analeta usawa na uwajibikaji kwa
watendaji wa Serikali.
Askofu Kilaini alisema hali ya sasa kwa utendaji wa Serikali imebadilika
kwani huko katika ofisi zaumma hakuna usumbufu wa kusubiria mtumishi,
wala hakuna ile tabia ya kuombwa kitu kidogo “Ile kauli ya unatuachaje
kama ilivyokuwa imezoeleka kwa baadhi ya watumishi katika sekta za umma
sasa haipo tena.”
Kilaini aliwataka Watanzania kutumia sherehe za mwaka mpya 2017
kujitathmini na kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza hasa kwa
mwaka uliomalizika 2016, hususani kama majanga ya tetemeko la ardhi
lililotokea Septemba 10 mwaka jana na kusababisha maafa makubwa mjini
Bukoba.
“Tetemeko lililotokea Kagera sio nyundo ya kuwahimiza,bali ni kengele ya
kutufanya tusonge mbele!hivyo,Watanzania tujielekeze kujituma kufanya
kazi na asiyefanya kazi hana sababu ya kula,kama yalivyo maandishi ya
kiroho,” alisema Askofu Kilaini.
Rais yuko mkoani Kagera kwa ziara yake ya siku mbili mkoani hapa pamoja
na shughuli zingine atakagua miradi mipya inayojengwa na kuweka mawe ya
msingi ambayo ni Shule ya sekondari ya Ihungo na zahanati ya Kabyaile
ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi na kuzungumza na wananchi wa
Kagera.
Post a Comment