BAADA YA KUENEA TAARIFA ZA KUYEYUKA KWA MABILIONI YA FEDHA KAGERA SERIKALI YAIBUKA
SIKU chache baada ya kuenea taarifa za kuyeyuka mabilioni ya fedha
yaliyochangwa na wasamaria wema kwa ajili ya kusaidia waathirika wa
tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Serikali imeibuka na kutoa taarifa juu
ya sakata hilo.
Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu,
aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi sasa Serikali imetumia Sh
bilioni 1.13 kukarabati miundombinu na si kuwajengea au kukarabati
nyumba wananchi ambao wanaishi kwenye mahema.
Aidha, Meja Jenerali Kijuu aliendelea kushikilia msimamo wa Serikali
kuwa kila mwananchi aliyeathirika na tukio hilo, ajihudumie na
kukarabati nyumba yake mwenyewe.
Alisema Serikali tayari imekusanya Sh bilioni 5.428 kutoka kwa watu,
taasisi na mashirika mbalimbali, waliotikia wito wa kusaidia waathiria
wa tetemeko hilo lililotokea Septemba 10, mwaka huu.
Kijuu alisema fedha hizo zilivunwa kupitia akaunti maalumu ya maafa
iitwayo ‘Kamati Maafa Kagera’ na michango mingine kupitia mihamala ya
fedha ya simu za mkononi.
Baada ya taarifa ya Kijuu kutoka, iliibua maswali na mjadala mkali, hasa
katika mitandao ya kijamii, ambako wachangiaji wengi walihoji kwanini
fedha hizo hazijawafikia walengwa hadi sasa, huku wakibaki kutaabika.
Kutokana na mjadala huo kushika kasi kila kukicha, jana Katibu Mkuu
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), Uledi Mussa, alilazimika
kutoa ufafanuzi wa Serikali namna ambavyo imeshirikina na wadau kuchukua
hatua kubwa za kuwasaidia waathirika na kwamba bado inaendelea kufanya
hivyo.
Alisema hadi kufikia Novemba 13, mwaka huu, Serikali ilikuwa imepokea
misaada ya vifaa, vyakula, fedha na ahadi mbalimbali zenye thamani ya Sh
bilioni 15.19.
Mussa alisema pamoja na misaada hiyo, tayari Serikali imetoa matibabu
bure kwa majeruhi wote 560, imeandaa na kugharamia mazishi ya watu 17
waliofariki dunia katika tetemeko hilo, huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
alihudhuria.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau ilitoa mkono wa pole wa Sh milioni
1.8 kwa kila familia iliyopatwa na msiba. Imeendelea kutoa misaada
mbalimbali ya kibinadamu ikiwamo chakula, dawa, nguo, makazi ya muda,
huduma za tiba, vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa kisaikolojia kwa
waathirika katika wilaya zote za Mkoa wa Kagera zilizopata athari,”
alisema.
Alisema Serikali imeendelea kufanya tathmini ya pamoja ya mahitaji ya
haraka ya athari za tetemeko hilo ili kubaini maeneo zaidi ya kuwasaidia
wananchi kwa kushirikiana na ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa
Mataifa na wadau mbalimbali, wakiwamo Msalaba Mwekundu, Plan
International (T), BRAC(T), World Vision, CARITAS, Save the Children, JH
Piego na Benki ya Dunia.
“Tathmini za wataalamu, makadirio ya awali yanaainisha Sh bilioni 104
zinahitajika kukabiliana na kurejesha hali katika Mkoa wa Kagera.
Gharama hizo zinajumuisha ujenzi wa makazi ya muda kwa waathirika wa
nyumba zipatazo 16,667 zilizoharibika katika viwango tofauti, ambapo
kiasi cha Sh bilioni 41.7 zinahitajika.
“Sh bilioni 1.92 kwa ajili ya kodi ya miezi sita kwa wapangaji waliokuwa
wakiishi kwenye nyumba zilizoharibika, ukarabati wa shule za msingi 163
kwa gharama ya sh bilioni 12.7, sekondari 57 kwa gharama ya Sh bilioni
45.65, vituo vya afya na zahanati 32 kwa gharama ya Sh milioni 772 na
majengo ya taasisi nyingine 20 kwa Sh bilioni 1.3,” alisema.
Alisema hadi kufikia Novemba 13, mwaka huu, Serikali imepokea misaada ya
vifaa, vyakula, fedha na ahadi mbalimbali zenye thamani ya Sh bilioni
15.19 kutoka kwa wadau mbalimbali, washirika wa maendeleo, balozi na
nchi marafiki. Tayari misaada hiyo imeshagawiwa na inaendelea kusambazwa
kwa walengwa.
“Mchanganuo wa misaada hiyo iliyopelekwa ipo kama ifuatavyo: Fedha
taslimu kiasi cha Sh 5,412,984,934.82 kimeshapokelewa kupitia benki.
Kiasi cha Sh 17,579,427.00 kupitia mitandao ya simu, ahadi za Sh
6,703,000,000. Hivyo jumla ya ahadi na fedha taslimu hadi sasa ni Sh
12,133,564,361.82,” alisema.
Alisema Serikali pia imepokea misaada mingine yenye thamani ya Sh
bilioni 2.25, ikiwamo unga tani 58.12, sukari mifuko 1,150, mchele tani
133.96, maharage tani 19,666, mahindi tani 70.1, majani ya chai tani 3,
maji katoni 1,570, mafuta lita 6,022, sabuni katoni 443, shuka 495,
blanketi 6,125, magodoro 1,146, mahema 367 na turubai 6,237.
Aliongeza: “Serikali imepokea pia vifaa vya ujenzi vikiwamo saruji
mifuko 24,233, bati 20,933, misumari kilo 145, nondo vipande 725, kofia
za bati 150 na mbao 250.
“Ifahamike baadhi ya waliotoa ahadi kama Serikali ya Uingereza,
wameahidi kutekeleza ahadi zao kwa kujikita moja kwa moja katika ujenzi
wa shule, baada ya Wakala wa Majengo kuainisha viwango na gharama. Aidha
Serikali inaendelea kupokea michango kutoka kwa wananchi na wadau
mbalimbali kwa lengo la kusaidia waathirika hawa.”
HATUA ZA KUREJESHA HALI
Mussa alisema tangu kutokea kwa maafa hayo, Serikali imeendelea kufanyia
kazi masuala muhimu yaliyoainishwa katika tathmini ya tetemeko.
Alisema hadi kufikia Novemba 13, mwaka huu, licha ya kuendelea kuwapatia
wananchi mahitaji muhimu kama chakula, dawa na misaada ya kujikimu
katika makazi ya muda, kiasi cha Sh 969,238,326.35, mifuko ya saruji
17,423, bati 5,348 na misumari kilo 1,107 vilitumika kwa kufanya
ukarabati mkubwa na mdogo wa shule za msingi na sekondari.
“Juhudi hizi ziliwezesha wanafunzi wa shule hizo waliokuwa katika hatari
ya kukosa masomo kuendelea na masomo yao. Gharama hizo pia zimejumuisha
ukarabati wa zahanati katika halmashauri za Mkoa wa Kagera, na kuanza
kwa ujenzi wa kituo kipya cha afya (Ishozi/Kabyaile) kitakachojumuisha
chumba cha upasuaji na wodi ya kinamama na watoto kwa faida ya wananchi
wote wa maeneo hayo.
“Pia Serikali imegharamia urejeshwaji wa miundombinu ya barabara, maji,
na umeme katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa na tetemeko,” alisema.
Alisema Shirika la Word Vision kwa kushirikiana na Serikali tayari
limetoa mifuko ya saruji 2,300 yenye thamani ya Sh 39,000,000 kwa kaya
460 zilizobomokewa nyumba na zilizoonekana kuwa na uhitaji zaidi. Katika
awamu ya kwanza kila kaya ilipata mifuko mitano ya saruji.
“Na kwa sasa utekelezaji wa awamu ya pili umeanza, inatarajiwa kugawiwa
mifuko ya saruji 10,645 yenye thamani ya Sh milioni 164.9 kwa kaya
2,129. Tumeainisha pia kaya nyingine zilizoathirika zaidi zipatazo 370
za watu waliomo kwenye makundi maalumu (wazee, wajane na walemavu),
ambao watapatiwa vifaa vya ujenzi (mabati 20 na mifuko mitano ya saruji
kwa kila kaya) kukarabati nyumba zao,” alisema.
Aliongeza: “Serikali inapenda kusisitiza tena kwa wananchi, maafa ya
tetemeko hayakupangwa wala kutokea kwa nguvu za mwanadamu bali majanga
ya asili, hivyo wakati juhudi zikiendelea kusaidia zaidi pale
panapowezekana, wananchi wanaendelea kuombwa kufanya jitihada zao
binafsi za kurejesha makazi yao katika hali yake ya awali.
“Serikali inawapongeza wananchi wengi ambao tayari wameitikia wito wa
Rais Dk. John Magufuli aliyewaasa kuanza ujenzi wa nyumba zao kwa kuwa
Serikali isingeweza kumjengea nyumba kila mwathirika.
“Kwa sababu ingawa michango na misaada hii japo haijafikia lengo la Sh
bilioni 104.9 zinazohitajika kurejesha hali nzima ya Kagera, itaendelea
kutumika kwa uadilifu na uwazi kwa faida ya waathiria wenyewe,” alisema.
Tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo
vya watu 17, watu 252 walijeruhiwa, nyumba 840 zilianguka na nyingine
1,264 zilipata nyufa.

Post a Comment