Mheshimiwa Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Mwenyekiti wa SADC wa Kamati
ya Mawaziri ya Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC
Ministerial Committee of the Organ on Politics, Defense and Security
Cooperation – MCO) amewasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa
ajili ya kuongoza Ujumbe wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa SADC Troika
(Tanzania, Angola na Msumbiji) kwa dhumuni la kufanya Misheni ya Pili ya
kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini humo.
Misheni hii inafanyika kufuatia Azimio la Mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa SADC Troika Mbili uliofanyika Falme ya Swaziland tarehe 17
Machi, 2017. Mkutano huo uliagiza kufanyika kwa Misheni ya Pili ili
kuendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hali ya siasa nchini DRC
wakati ikifanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi
Desemba, 2017.
Sambamba na hayo, Viongozi Wakuu katika Mkutano huo walipokea na
kujadili taarifa ya hatua zilizochukuliwa na SADC katika kutatua
changamoto za kisiasa, kiulinzi na kiusalama katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ikiwemo Taarifa ya Misheni ya Kwanza ya Mawaziri
iliyofanyika mwezi Oktoba, 2016 na Taarifa ya Misheni ya Timu ya
Wataalam wa SADC nchini DRC iliyofanyika mwezi Februari, 2017.
Katika Misheni hii ya Pili, ujumbe wa Angola utaongozwa na Mhe.
Manuel Augusto, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje; na ujumbe wa Msumbiji
utaongozwa na Mhe. Nyeleti Mondlane, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Ratiba inaonyesha kuwa ujumbe wa Misheni ya Mawaziri wa SADC
utakutana na kufanya mazungumzo na wadau wafuatao: Serikali ya DRC
akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo; Wawakilishi wa Jeshi la
Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO); Wawakilishi wa Baraza la
Maaskofu Katoliki nchini DRC (CENCO); Wawakilishi wa Vyama vya Siasa na
Asasi za Kiraia; na Ofisi ya Rais – DRC. Aidha, Mawaziri watapata pia
fursa ya kufanya mazungumzo na Mabalozi wa nchi wanachama wa SADC wenye
makazi mjini Kinshasa.
Misheni inatarajiwa kukamilika tarehe 21 Aprili, 2017.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Home
»
habarizakitaifa
» Taarifa kuhusu misheni ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa SADC Troika nchini DRC
About Author
The part time Blogger love to blog on various categories like Web Development, SEO Guide, Tips and Tricks, Android Stuff, etc including Linux Hacking Tricks and tips. A Blogger Template Designer; designed many popular themes.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment