MASHINDANO YA MABALOZI WA MTOTO MFANYAKAZI WA NYUMBANI YAFANA JIJINI MWANZA.
Mgeni
rasmi, Afisa Ustawi wa Jamii mkoani Mwanza, Kizito Wambura (kulia),
akikabidhi kombe kwa washindi wa mashindano hayo yaliyofanyika leo
katika viunga vya shule ya msingi Nyamagana.
Wanafunzi
wa shule ya msingi Nyamagana wameibuka washindi kwenye mashindano
elimishi kwa klabu za mabalozi wa mtoto mfanyakazi wa nyumbani dhidi ya
wakubwa zao kutoka shule ya sekondari Nyakurunduma, zote za Jijini
Mwanza.
Mashindano
hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya kutetea haki za mtoto mfanyakazi wa
nyumbani (WoteSawa) ya Jijini Mwanza, yalijumuisha michezo mbalimbali
ikiwemo maigizo, ngonjera pamoja na mashairi yenye jumbe za kuainisha
aina za ukatili wanaokumbana nao watoto wafanyakazi wa majumbani ikiwemo
vipigo, utumikishwaji na fursa ya kukosa elimu, na kuiasa jamii
kuachana na vitendo hivyo.
"Ukiona
mtoto anatendewa ukatili wa aina yoyote, paza sauti (toa taarifa)
sehemu mbalimbali ikiwemo WoteSawa, polisi kupitia kitengo cha dawati la
jinsia, kwa Mwenyekiti wa Mtaa ama Mtendaji wa Kata". Amesisitiza mgeni
rasmi, Wambura.
Naye
Mkurugenzi wa taasisi ya WoteSawa, Angel Benedicto, amebainisha kwamba
bado watoto wafanyakazi wa majumbani wanakabiliwa na vitendo mbalimbali
vya ukatili ikiwemo kutumikishwa kwa kuajiriwa ili kutembeza bidhaa
mtaani kwa ujira mdogo, kunyimwa fursa ya kusoma pamoja na vipigo kutoka
kwa baadhi ya waajiri hivyo taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu katika
jamii ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.
"Lengo
ni kupunguza ukatili wa watoto majumbani, kulinda haki za watoto,
kuibua vipaji ikiwemo uchoraji na uigizaji ili kuvitumia katika
kufikisha elimu ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto". Imefafanua
sehemu ya risala ya klabu za wanafunzi mabalozi wa mtoto mfanyakazi wa
nyumbani kutoka shule ya msingi Nyamagana na Nyakurunduma sekondari,
iliyosomwa na Neema Christopher.
Shule
ya msingi Nyamagana wakifurahia ushindi wao ambapo igizo wamepata
asilimia 93 dhidi ya 92 za Nyamagana sekondari, Shairi Nyamagana
wamepata asilimia 74 dhidi ya 85 za Nyakurunduma huku Ngonjera Nyamagana
wakipata asilimia 91 dhidi ya 77 za Nyakurunduma. Ushindi wa jumla,
shule ya Msingi Nyamagana wamepata asilimia 86 dhidi ya 85 za
Nyakurunduma sekondari.
Mabalozi kutoka shule ya sekondari Nyakurunduma wakipokea kombe baada ya kushika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo
Pia mabalozi wote wamepatiwa vyeti kwa kujitoa kuwa mabalozi wa mtoto mfanyakazi wa nyumbani
Mabalozi wakipokea vyeti
Mabalozi kutoka shule ya msingi Nyamagana wakionesha makali yao katika ngonjera na mashairi
Mabalozi kutoka Nyakurunduma sekondari wakighani mashairi na ngonjera
Afisa Ustawi wa jamii Jijini Mwanza, Davis Justine (katikari) akitoa matokeo ya mashindano hayo kwa niaba ya majaji wengine
Mkurugenzi wa WoteSawa, Angel Benedicto, akizungumza wakati wa mashindano hayo
Diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha, akizungumza kwenye mashindano hayo
Taasisi
ya WoteSawa imechora mchhoro huu katika shule ya Msingi Nyamagana,
ukiwa na jumbe mbalimbali ikiwemo "Mpe elimu siyo kumuajiri kazi za
nyumbani" ikiwa ni mwendelezo wa kufikisha elimu juu ya mapambano dhidi
ya ukatili wa mtoto mfanyakazi wa nyumbani.
Mgeni rasmi akizungumza jambo kwenye mashindano hayo na kuzindua pia mchoro huo
Mabalozi
wa mtoto mfanyakazi wa nyumbani kutoka shule ya sekondari Nyakunduruma
Jijini Mwanza wakiwa na vyeti vyao walivyotunukiwa na taasisi ya
WoteSawa
Mabalozi
wa mtoto mfanyakazi wa nyumbani kutoka shule ya shule ya msingi
Nyamagana Jijini Mwanza wakiwa na vyeti vyao walivyotunukiwa na taasisi
ya WoteSawa
Mabalozi wote wakiwa kwenye picha ya pamoja
Post a Comment