MAKALA: WIKI YA SHERIA NA SIKU YA SHERIA NCHINI, 2017
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akikagua gwaride maalum
lililoandaliwa, ukaguzi wa gwaride hili huashiria kuanza rasmi kwa
shughuli za Mahakama kwa mwaka husika.
Na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania
Nchi
yoyote yenye kuzingatia misingi ya Utawala wa Sheria, huchangia kwa
kiasi kikubwa kuleta amani na Maendeleo ya kiuchumi katika taifa husika.
Hii
inajidhihirisha kupitia Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria
nchini, 2017 ambayo ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha
Ukuaji wa Uchumi.’
Kauli
mbiu hii ina maana ya kuwa kukamilishwa mapema kwa mashauri ya jinai,
Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo yanaendeleza amani na usalama katika
jamii ni chachu ya maendeleo ya uchumi.
Hivi
karibuni Mahakama ya Tanzania iliadhimisha Siku ya Sheria nchini, ambayo
huashiria kuanza rasmi kwa mwaka wa Mahakama ambapo shughuli za
usikilizaji wa Mashauri huanza rasmi.
Kwa
mwaka huu, sherehe za Siku ya Sheria nchini ziliadhimishwa rasmi tarehe
02.02.2017, ambapo kila Mkoa uliadhimisha, kwa upande wa Dar es Salaam,
Sherehe hizi zilifanyika katika Kiwanja cha Mahakama kilichopo Chimala
karibu na Hospitali ya ‘Ocean road’ ambapo Mgeni rasmi alikuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
akihutubia watumishi na wageni waalikwa katika Siku ya Sheria nchini
iliyofanyika Februari 02, 2017.
Aidha;
Sherehe za Kilele cha Siku ya Sheria nchini zilitanguliwa na Maonyesho
ya Wiki ya Sheria yaliyoanza rasmi Januari, 28 hadi Februari 01, 2017,
Maonyesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika nchi nzima lengo kuu likiwa ni
kutoa elimu ya Sheria kwa Wananchi juu ya huduma na taratibu mbalimbali
za Kisheria.
Kwa
upande wa Dar es Salaam, Maonyesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini humo, Wadau walioshiriki ni pamoja
Mahakama yenyewe kama mwenyeji, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama
Kuu Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Mahakama (AGC), Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo cha Uongozi
wa Mahakama IJA, Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Huria, Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Wengine
ni Tume ya Kurekebisha Sheria, Taasisi zinazotoa msaada wa Kisheria
(Legal Aid), TAKUKURU (PCCB), Polisi, Magereza, Msajili, Mabaraza ya
Ardhi, Chama cha Wanasheria
Tanganyika
(TLS), Tume ya Kurekebisha Sheria, Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA, Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Chama cha
Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Sekretarieti ya Msaada wa Sheria,
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ‘Tanzania Network of Legal Aid
Provider (TANLAPS),’ Legal Aid and Human Centre na NHIF.
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma akisoma risala yake
ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 02, 2017, waliopo nyuma
ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu ni baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya
Tanzania.
Katika
maonesho hayo kulikuwa na uwakilishi wa ngazi zote za Mahakama kuanzia
Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufaa ambapo taratibu/huduma
mbalimbali za Kimahakama zilitolewa kwa wananchi waliopata fursa ya
kutembelea mabanda ya Maonesaho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Lengo
la kufanyika kwa Maonesho hayo ilikuwa ni kutoa fursa kwa wananchi
kufahamu shughuli za Mahakama pamoja na Wadau wa Sekta Sheria kwa
ujumla, vilevile kuwawezesha wananchi kupata elimu juu ya taratibu
mbalimbali Mahakama katika upatikanaji wa haki.
Aidha,
Sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini zilihudhuriwa na Wageni
mbalimbali akiwepo Spika wa Bunge la Tanzania, Waziri wa Katiba na
Sheria, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakuu wa
Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Mwendesha Mashtaka (DPP), TLS,
Majaji Wastaafu, Mabalozi, Viongozi wa dini mbalimbali n.k.
Aidha katika Sherehe hizo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumzia masuala kadhaa ambayo ni pamoja na:-
Kutoa
pongezi kwa kasi nzuri ya Uondoshaji wa Mashauri, ambapo katika taarifa
iliyotolewa na Kaimu Jaji Mkuu alisema kuwa ‘Pamoja na changamoto
inayotukabili ya uwiano usio sawa wa idadi ya Majaji na Mahakimu na
Watumishi wengine kama Wasaidizi wa Kumbukumbu; wastani wa jumla ya
umalizaji wa mashauri upo wa asilimia 101 (101%), yaani kwa tafsiri ya
kila mashauri mia moja (100) yanayosajiliwa uwezo wa kuyamaliza ni
asilimia 101 (101%).
Kwa
mwaka wa Mahakama ulioisha Desemba, 2016, jumla ya mashauri 276,147
yalisajiliwa na mashauri yaliyosikilizwa na kukamilika yalikuwa ni
279,331.
Viongozi
wanaoiwakilisha Mihimili mitatu ya Dola wakiwa katika picha ya pamoja
katika Siku ya Sheria nchini, wa pili kushoto ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, wa kwanza kushoto
ni Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji, Prof. Ibrahim Juma, wa pili
kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job
Ndugai na wa kwanza kulia, Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Ferdinand Wambali.
Mashauri
ambayo yapo bado Mahakamani ilipofika Desemba, 2016 ni jumla 56,531 na
kati ya hayo, yenye sifa ya kuitwa ya zamani (backlogs) ni mashauri
3,618 na ambayo ni sawa na wastani wa asilimia sita (6%) tu.
Mhe.
Prof. Jaji Juma aliongeza kuwa kati ya mashauri 249 yaliyosajiliwa
Mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi ambapo ya Ubunge yalikuwa 53 na
Udiwani 196. Hadi kufikia Desemba 30, 2016 mashauri 52 yaliyohusu ubunge
yaliamuliwa, hivyo kubaki na shauri moja (1) tu. Mashauri ya udiwani
yalisikilizwa na kuamuliwa yote. Mashauri ya uchaguzi wa Ubunge
yalisikilizwa mfululizo kuanzia mwezi Juni mpaka Oktoba, 2016
yakijumuisha Majaji 29 kwa yale ya Ubunge; na Mahakimu kwa mashauri ya
Udiwani.
Ari
hii ya Kasi ya usikilizwaji wa Mashauri mbalimbali, ilimfurahisha Mhe.
Rais na kupelekea kutoa pongezi kwa Mahakama kwa kazi nzuri waliofanya
katika mwaka wa Mahakama uliopita.
Mbali
na pongezi, Mhe. Rais alitoa changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na
‘Mashauri ya kodi na fedha zilizokwama kutokana na wadaawa na masjala za
Mahakama kufanya mchezo maarufu wa ‘Parking’ kuzuia mashauri
yasimalizike na kuikosesha serikali mapato.’ Katika hili Mhe. Rais
aliiomba Mahakama kutilia mkazo katika mashauri haya ili kuingizia
Serikali mapato.
Baadhi
ya Watumishi wa Mahakama na Wageni wengine waalikwa wakiwa katika
sherehe za Siku ya Sheria nchini, iliyofanyika Februari 02, 2017.
Hata
hivyo; Mahakama pamoja na jukumu lake kuu la kutoa haki,imekuwa mstari
wa mbele katika kuhakikisha nchi inajenga na kuweka mazingira bora ya
biashara shindani ili kuvutia uwekezaji.
Kwa
upande wake, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma,
katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini, alisema kuwa Mahakama ya
Tanzania imedhamiria kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha wadaawa wanapata
nakala ya hukumu ndani ya siku 21 na mwenendo wa shauri ndani ya siku
30 tangu hukumu iliposomwa.
“Wananchi
wanastahili kupata nakala za hukumu kwa wakati. Sheria inataka kila
Jaji au Hakimu asome hukumu ndani ya siku 90 tangu kesi ilipomalizika
kusikilizwa,” alisisitiza Kaimu Jaji Mkuu.
Miongoni
mwa masuala ambayo Kaimu Jaji Mkuu aliyatilia msisitizo/mkazo katika
hotuba yake pia ni pamoja na matumizi ya TEHAMA Mahakamani ili
kurahisisha taratibu mbalimbali za Mahakama.
“Ifikapo
Desemba, 2018, kulingana na ramani (Road map) ya matumizi ya TEHAMA,
kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (E-govt Agency), tuweze
kuanza matumizi kamili ya TEHAMA kwenye kazi za Kimahakama na
Kiutawala,” alisema Jaji Juma.
Aliongeza
kuwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kisasa ya Mahakama pia
unaenda sanjari na matumizi ya hatua kwa hatua ya TEHAMA, vilevile
kuhakikisha taratibu za masuala ya fedha ndani ya Mahakama zinaendeshwa
kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA mpaka kwenye ngazi ya
Mikoa/Wilaya.
Alienda
mbali na kuongeza kuwa Mfumo wa TEHAMA wa ukusanyaji wa Takwimu za
Mashauri (JSDS) utaboreshwa kuwa sehemu ya mfumo wa kisasa. Matumizi
makubwa ya Watanzania ya simu za kisasa (smart phone) yanarahisisha sana
azma hii ya kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji kazi wa kizamani na
wenye tija hafifu.
Jitihada
mbalimbali zifanywazo na Mahakama kwa sasa kama ujenzi na ukarabati wa
miundombinu, matumizi ya TEHAMA n.k zinalenga katika kuboresha na
kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Naye,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. George Masaju katika hotuba yake ya
Siku ya Sheria nchini aliitaka Mahakama kukamilisha mapema mashauri ya
jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo yanaendeleza amani na usalama
katika jamii ni chachu ya maendeleo ya uchumi.
“Majaji,
Wasajili, Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na
wadau wengine wa Mahakama, ikiwemo vyombo vya upelelezi wa jinai, Rushwa
na Uhujumu uchumi, Mabaraza ya kodi, Ardhi, Ushindani na mengineyo
wazingatie matakwa ya Katiba ya nchi, Sheria na Kanuni katika utoaji
haki kwa wakati,” alieleza Masaju.
Siku
ya Sheria nchini, hutoa nafasi kwa Mahakama pamoja na wadau wake wakuu
ambao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Chama cha
Mawakili Tanganyika kutoa hotuba juu ya Mafanikio na changamoto
zinazoikabili Sekta ya Sheria katika mwaka husika.
Kwa
upande wake Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Bw. John Seka
aliihakikishia Mahakama kupitia hotuba yake kuwa Chama hicho kipo tayari
wakati wowote kushirikiana na Mahakama ili kuhakikisha kuwa utoaji haki
unatamalaki.
Maadhimisho
ya Siku ya Sheria nchini hutumika kama njia mojawapo ya kukutana na
Wadau ili kupata michango/maoni mbalimbali ya Wadau na wananchi kwa
ujumla yote yakitumika na Mahakama kujitathmini na kuona wapi imepwaya
ili kuendelea kufanya maboresho katika suala zima la utoaji haki nchini.
Akiongea
na Mwandishi wa Makala hii, Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Katarina Revocati alisema kwa mwaka huu mpya wa Sheria, Mahakama
imejipanga kuhakikisha inaendelea kushughulikia mlundikano wa
kesi/mashauri ya muda mrefu ‘case backlog’.
“Kama
unavyojua kwa sasa, Mahakama imejikita katika kufanya maboresho kadhaa
wa kadhaa, miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na kushughulikia
mashauri ya muda mrefu, na jitihada hizi zimezaa matunda hata kwa mwaka
jana ambapo hadi tunamaliza mwaka tulikuwa mlundikano sifuri (zero
cases) katika ngazi za Mahakama za Mwanzo na za Wilaya,hivyo jitihada
hizi zinaendelea hata kwa sasa,” alieleza Mhe. Revocati.
Msajili
Mkuu huyo aliendelea kusema kuwa Mahakama imejiwekea muda maalum wa
kushughulikia kesi hadi kumalizika kwake, ambapo alieleza kuwa kwa ngazi
ya Mahakama za Mwanzo kesi inabidi iwe imekamilika kwa kipindi cha
miezi sita, Mahakama za Wilaya/Hakimu Mkazi, mwaka mmoja na kwa upande
wa Mahakama Kuu/Rufani miaka miwili (2), na suala hili tunalisimamia
kwani pia Mpango Mkakati wetu wa Mahakama kupitia moja ya nguzo zake
inaelekeza kuboresha suala zima la utoaji haki nchini.
Mahakama
ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria nchini ndani ya wiki ya kwanza
wa mwezi Februari kila mwaka, siku hii huashiria mwanzo wa shughuli za
Mahakama kwa mwaka husika, maudhui ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na
Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa
wakati kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.’
Kwa
mara ya kwanza, Mahakama ya Tanzania iliadhimisha rasmi Siku ya Sheria
nchini mwaka 1997 ambapo Viongozi wa Dini walitoa dua ya kuombea Majaji,
Mahakimu na Wanasheria ili watimize wajibu wao mzito wa utoaji haki
nchini. Hata hivyo mnamo Machi 1, 1996 kulifanyika ibada maalum ya
kuwaombea Majaji na Mahakimu ili wasikilize vyema mashauri yoyote na
hasahasa ya uchaguzi Mkuu uliofanyika 1995. Huu ulikuwa uchaguzi wa
kwanza wa vyama vingi na hivyo kulikuwa na mashauri mengi ya uchaguzi.
Aidha;
mnamo mwaka 2007, Sherehe za Siku ya Sheria nchini zilihudhuriwa na
Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza na Mheshimiwa Rais alipata nafasi ya
kutoa hotuba na huu ndio ulikuwa mwanzo wa mgeni rasmi kutoa hotuba.
Post a Comment