AFISA MTENDAJI AUAWA KWA KUBANWA PUMZI MBEYA
Mwili wa ofisa mtendaji wa mtaa wa Kabwe, katika kata ya Iyela jijini
Mbeya Clementine Enock (34) umekutwa ukiwa umetelekezwa katika eneo la
Airport ya zamani baada ya kuuawa na watu wasiofahamika kwa kubanwa
pumzi.
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa
walibaini kuwepo kwa mwili huo Januari mbili, mwaka huu majira ya saa
moja asubuhi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Kidavashari alifafanua kuwa kabla ya tukio hilo marehemu aliondoka
nyumbani kwao siku ya Mwaka mpya na kuaga kuwa anakwenda Airport kwenye
sherehe ya rafiki yake huku akiwa na gari yenye namba za usajili T234
DJM aina ya Toyota Spacio.
Alisema kuwa ndugu wa marehemu walipata hofu mara baada ya ndugu yao
kuchelewa kurudi nyumbani na ndipo wakaanza kumpigia simu bila mafanikio
mpaka usiku wa manane.
“Marehemu aliaga nyumbani kwao Uyole ya Kati alikokuwa akiishi majira ya
saa kumi jioni siku ya tarehe moja kwa madai anaenda kwenye sherehe ya
rafiki yake akiwa na usafiri wa gari lake, ambapo mpaka kufika usiku wa
manane hakukuwa na taarifa yeyote ndipo hofu ikatanda kwa familia ambapo
walipiga simu kwa ndugu jamaa na marafiki na kueleza kuwa hawajui
alipo,” alisema Kidavashari.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari siku iliyofuata majira ya saa moja
asubuhi mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umetupwa katika eneo la wazi
jirani na Shule ya Sekondari ya Samora ambapo uchunguzi wa awali
unaonesha kifo chake kilitokana na kubanwa pumzi na watu wasiofahamika.
Alisema mazingira ya kifo yanaonyesha wazi kuwa marehemu aliuawa na mtu
wa karibu yake huku akisema tukio hilo lilifanywa ndani ya nyumba ya
mtu.
Post a Comment