TRUMP AKATAA KUCHUKUA MSHAHARA WA URAIS MAREKANI
Rais mteule wa Marekani, bilionea Donald Trump amesema hatakubali kupokea mshahara wa urais pindi atakapokuwa madarakani.
Trump ameweka msimamo huo jana katika mahojiano maalum na mtangazaji
maarufu, Lesley Stahl katika kipindi cha 60 Minutes, aliyetaka kufahamu
kuhusu uamuzi wake juu ya mshahara wake akiwa ni mfanyabiashara mkubwa.
“Sijawahi kuzungumzia hili, lakini jibu langu ni hapana,” alisema.
“Nafikiri inanibidi kupokea kwa mujibu wa sheria $1, kwahiyo ntachukua
$1 (Sawa na shilingi 2,200 za Tanzania) kwa mwaka. Lakini hata sijui ni
nini,” aliongeza.
Ingawa mtangazaji huyo alimkumbusha Trump kuwa anaiacha $400,000 kwa
mwaka, rais huyo mteule alisisitiza, “sitachukua mshahara. Sitapokea.”
Wakati wa kampeni, Trump aliahidi kuwa atajiweka kando na biashara zake
endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani, na kwamba atajikita zaidi
katika kutimiza ahadi zake kwa Wamarekani. Alisema kuwa biashara zake
ataziacha mikononi mwa watoto wake.

Post a Comment