DC HAPI AFUNGUA RASMI MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA VIJANA WA KINONDONI
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Ally Hapi leo jumatatu tarehe 14/11/2015
amefungua rasmi mafunzo ya ujasiliamali kwa awamu ya kwanza.
Katika
Uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya amewata Vijana kuondokana na mawazo ya
kuajiriwa pindi wanapohitimu vyuo vya Elimu ya juu na hata wale wasio na
elimu hiyo, bali wajikite kutumia fursa zilizopo kujiajiri jambo ambalo
litawasaidia kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira na kujenga uchumi
wao na wa taifa.
Hayo
yamebainishwa leo na mkuu wa wilaya ya kinondoni, Ally Hapi wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya ujasiliamali wilaya ya Kinondoni kwa lengo la
kuwajengea uwezo wa kubuni, kuanzisha na kusimamia biashara na miradi
mbalimbali.
Hapi
amesema kuwa hakuna serikali duniani yenye uwezo wa kuajiri watu wake
wote wenye uwezo wa kufanya kazi kutokana na ufinyu wa nafasi za ajira
kulinganisha na mahitaji halisi. Bali wanaweza kujenga maisha yao kwa
kubadilisha fikra na kuamua kujiajiri katika vikundi.Amesema,
kuwa jukumu la serikali ni kuwawekea sera, mikakati na mazingira mazuri
kwa vijana ili waweze kujiari katika shughuli za ujasiriamali.
"Kazi
tunayoifanya hapa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ambayo
inaeleza wazi jukumu la serikali ya awamu ya Tano katika kuwasaidia
vijana wa elimu tofauti kujiajiri na kufanya shughuli za ujasiriamali
katika vikundi. Tumeanza na awamu hii ya kwanza itakayonufaisha vijana
elfu moja, na tutaendelea na awamu nyingine hadi tumalize vijana wote
elfu kumi waliojiandikisha."
Alisema Hapi.
Hata
hivyo, DC Hapi amesema ameanzisha mafunzo hayo kwa nia ya kuwaondoa
uwoga vijana na kuwajengea ujasiri na uthubutu katika kuamua kujiajiri
kwani amebaini vijana wengi na hasa wanaohitimu vyuoni ni wazito na
waoga kujiajiri, jambo ambalo ameeleza kuwa linatokana na mfumo wa elimu
kujikita katika nadharia zaidi kuliko kuwaandaa vijana kifikra na
kivitendo kuanzisha shughuli zao binafsi za kiuchumi.
"Rais
wetu Dr. John Magufuli ameahidi kupitia Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi kuwa mikopo itatolewa katika ngazi ya mitaa na vijijini ili
kuwawezesha vijana kujiajiri katika vikundi. Sisi kama Kinondoni
tumeamua kujiandaa kwanza kwa kutoa mafunzo kwa watu wetu. Ili wajue
nidhamu ya kukopa, kulipa deni, kubuni wazo la biashara, kuanzisha na
kusimamia biashara na kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi wao.
Hatutaki
vijana wetu wakope fedha hizo wakiwa hawajapata elimu ya kutosha
kuwawezesha kufanya ujasiriamali wa kisasa. Matokeo yake fedha
zitatolewa na zitashindwa kuleta matunda yaliyokusudiwa."
Alisema Mh. Hapi
Kwa
upande wao vijana ambao wameanza mafunzo hayo leo wamemshukuru Mkuu huyo
wa wilaya huku wakihaidi kuitumia elimu watakayopewa kujenga maisha yao
na uchumi wa taifa.
Vijana
wapatao 10,000 walijitokeza kuitikia wito wa kampeni iliyoanzishwa na
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mapema mwezi June ambao watapatiwa
mafunzo ya ujasiriamali bure ili kujiandaa kukabiliana na tatizo la
ukosefu wa ajira nchini. Awamu hii ya mafunzo inajumuisha washiriki 1000 kwa uwakilishi kutoka kila kata katika kata 20 za Kinondoni.
Mafunzo
hayo yamefunguliwa katika ukumbi wa king solomon Namanga jijini Dar es
salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka benki ya NMB, PPF,
Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi NEEC n.k.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally Hapi akisalimiana na Mkufunzi wa Ujasiriamali Bi. Debora Charles (kushoto) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wajasiriamali vijana wa Manispaa ya Kinondoni jana Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally Hapi akizungumza na vijana wajasiriamali wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wajasiriamali vijana wa Manispaa ya Kinondoni jana Jijini Dar es Salaam.

Mkufunzi wa Ujasiriamali Bi. Debora Charles akitoa mada wakati wa mafunzo ya wajasiriamali vijana kutoka Manispaa ya Kinondoni jana Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali kutoka Manispaa ya Kinondoni wakifuatilia mafunzo ya ujasiriamali wakati wa mafunzo hayo jana Jijini Dar es Salaam.

Post a Comment